Maafisa kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, Makamanda  na Wakuu wa Polisi kutoka Mikoa ya  (Dar es salaam, Pwani, Lindi na Mtwara) inayopitiwa na bomba la gesi asilia wamefanya ziara ya kutembelea miundombinu ya gesi asilia iliyoko Mnazibay na kiwanda cha kuchakata gesi cha Madimba mkoani Mtwara.

Ziara hiyo iliyoandaliwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kupitia Kampuni Tanzu (GASCO) ikiwa na  lengo la Makamanda hao kujionea hali halisi ya ulinzi na usalama wa miundombinu ya gesi asilia  wanayoilinda na kuisimamia.

Akizungumza katika ziara hiyo Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi ACP.Philip Kalangi, amewasisitiza Makamanda wa Jeshi la Polisi  kuendelea kuboresha ulinzi kwenye miundombinu ya gesi asilia ambayo inapita kwenye maeneo wanayoyasimamia pamoja na  kuimarisha usimamizi kwa Maaskari wanaowasimamia.

Aidha, Mkuu wa Kitengo cha Usalama GASCO Bw. Fred Mfikwa amesema, TPDC inaendelea kujenga uhusiano na ushirikiano na Jeshi la Polisi pamoja na Viongozi na Wanachi wa Vijiji  vinavyopitiwa na bomba ili kuhakikisha miundombinu ya gesi asilia inakuwa salama wakati wote.

Bomba la gesi asilia kutoka Mtwara hadi Dar es salaam lina urefu wa kilometa 551 na limepita katika Vijiji 139.