Nyumba 570 Zaunganishwa na Mtandao wa Gesi Asilia Dar es salaam

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limeendelea na utekelezaji wa miradi ya kusambaza gesi asilia ambapo nyumba 570 za maeneo ya Sinza na Kota za Polisi Kurasini jijini Dar es Salaam zimeunganishwa na mtandao wa gesi asilia.

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dkt. James Mataragio alisema, “ tumekamilisha mradi huu wa nyumba 570 ambao unaongeza idadi ya watumiaji wa gesi asilia majumbani kufikia zaidi ya 2000”. Dkt. Mataragio pia alieleza kuwa miradi ya kusambaza gesi asilia majumbani ni miradi endelevu ambayo kila mwaka TPDC inatenga fedha katika bajeti zake kwa ajili ya kutekeleza miradi ya namna hii na kwa mwaka ujao wa fedha 2022/23 TPDC imetenga zaidi ya Shilingi Bilioni 20 kwa ajili ya miradi ya kusambaza gesi asilia majumbani.

Kwa upande wake Meneja Mradi kutoka TPDC, Mhandisi Angilindile Marandu alisema mradi huu umegharimu Shilingi Bilioni 2.14 na umetekelezwa na mkandarasi mzawa. Mhandisi Marandu alifafanua pia kuwa mradi huu ulipaswa kukamilika mapema mwaka huu lakini changamoto za UVIKO-19 ziliathiri mnyororo mzima wa usafirishaji  mizigo duniani na hivyo kuathiri  mradi huu kupata vifaa kwa wakati.

Nae Bi. Assenga ambaye ni mteja katika Kota za Polisi Kurasini alieleza kuwa anafurahia kutumia gesi asilia kwani inampa unafuu wa gharama, “gesi hii ni nzuri kwani naweza kununua hata ya shilingi 3000 nikatumia tofauti na ile ya mitungi ambayo lazima ulipie mtungi mzima.”