Dodoma,

Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amesema anataka kuona Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) linakuwa Shirika la kimkakati nchini ili kwa miaka ijayo shughuli zote za kuchakata na kusindika gesi asilia zifanywe na Shirika hilo.

Rais Samia alisema hayo Juni 11,2022 wakati wa hafla ya utiaji Saini makubaliano ya awali ya mkataba wa nchi hodhi wa mradi wa kusindika gesi asilia  kuwa kimiminika (LNG), ambapo ameiagiza Wizara ya Fedha na Mipango pamoja Wizara ya Nishati kukaa na kujadiliana kuona namna ya ushiriki wa TPDC katika mradi huo unakuwa wa tija na manufaa makubwa zaidi.

Rais Samia aliiagiza TPDC kuanza mara moja kujenga uwezo wa Watanzania kushiriki kikamilifu na kutumia manufaa yatokanayo na mradi huo na kwamba mradi mkubwa lazima ulindwe, walindaji wakubwa ni sisi na sio Wawekezaji.

Rais Samia alitoa maelekezo kuendelea kusimamia maslahi ya nchi kwenye hatua ya mazungumzo yanayoendelea kuhusu mradi huo na kutambua kwamba katika majadiliano hawawezi kukubaliwa kila unachokitaka hivyo wawe na uwezo wa kubadili mawazo kutokana na maongezi yatakayokuwepo.

” Huu ni mradi mkubwa na wa kimkakati kwa nchi yetu, tumekuwa na miradi mingine ya kimkakati kwa miaka ya hivi karibuni lakini yote ni sisi tunatoa mitaji na kutumia katika miradi lakini mradi huu una umahususi wake kwa sababu unaleta mtaji na unaleta mapato nchini” alisema Rais Samia.

Aidha Rais Samia alizitaka sekta binafsi kuanza kujipanga kuchukua nafasi za kutoa huduma kwenye mradi huo na wananchi pia ili kukuza uchumi wa ndani kuliko kuwaachia watu wa nje waje watoe huduma na mapato yaende kwao.

Halikadhalika, Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba alisema hadi kufikia mwezi Mei, 2022, jumla ya futi za ujazo trilioni 57.54 za gesi asilia ziligunduliwa katika maeneo mbalimbali ya nchini na kati ya hizo, jumla ya futi za ujazo trilioni 47.13 ni katika vitalu vilivyopo katika kina cha bahari na futi za ujazo trilioni 10.41 ni katika maeneo ya nchi kavu, ugunduzi wa kiasi hicho kikubwa cha gesi asilia ulifanyika kwa ushirikiano wa Serikali na Makampuni.

Mhe. Makamba alisema utekelezaji wa mradi huo katika Mkoa wa Lindi utafanyika sambamba na uendelezaji wa miundombinu kwenye mkondo wa juu ili kuwezesha kuvuna rasilimali hiyo, na kwamba Mradi huo utabadilisha sura na taswira ya uchumi wa nchi.

Alisema eneo ambalo mtambo utajengwa tayari limeshajulikana na kuwekwa katika miliki ya Serikali kwa kuwalipa fidia ya takriban Shilingi Bilioni 5.71 wananchi 642 waliokuwa wakazi wa maeneo hayo.

Mhe. Makamba alisema baadhi ya manufaa ya mradi huo ni kuchochea ukuaji wa uchumi, kuiongezea Serikali Mapato, kuongeza ajira na kuongeza uwezo wa Watanzania kitaaluma.

Naye, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba alisema utiaji saini huo unaweka msingi mkuu wa kukamilisha majadiliano ya mkataba wa ‘’Host Government Agreement’’ na mikataba mingine ya utekelezaji wa mradi wa kuchakata gesi asilia ambapo tunatarajia mazungumzo hayo kuendelea hadi Disemba, 2022.

Kwa upande wao wawakilishi wa Makampuni ya Kimataifa ya Mafuta, Jared Kuehi, Makamu wa Rais na Meneja Mkazi wa Kampuni ya Shell na Unni Fjaer, Meneja Mkazi wa Kampuni ya Equinor walisema wanatambua jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuweka kipaumbele katika mradi huo, huku wakishukuru kwa nafasi waliopatiwa kufanya kazi na Waziri Makamba pamoja na Viongozi wengine wa Serikali.

Uwekezaji katika mradi huu unatarajiwa kugharimu takriban Shilingi Trilioni 70, kwa mujibu wa tafiti, asilimia 10 ya kiasi hicho kitatumika ndani ya nchi katika kipindi ambacho mradi unajengwa. 

Fedha hizo zitatumika katika ununuzi wa vifaa na kutoa huduma za ndani ya nchi ikiwemo huduma za usafirishaji, ukodishaji wa mitambo, chakula, ulinzi, bima na malazi.