Mkurugenzi Mtendaji  wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Bw. Mussa Makame amesema TPDC imejipanga kuhakikisha gesi asilia inayozalishwa Nchini

kwaajili ya kuzalisha nishati ya umeme majumbani  unatumika kwenye matumizi mengine ikiwemo uendeshaji wa magari.

Bw. Makame amesema hayo tarehe 20/07/2023 Jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano na Wahariri wa Vyombo vya Habari kwa lengo la kujadili mafanikio na mikakati  mbalimbali ya Shirika kwenye utekelezaji wa miradi ya kuongeza upatikanaji wa mafuta na gesi asilia pamoja na kasi ya usambazaji.

Makame amesema mkakati wa Shirika ni  kuendelea kujenga mabomba ya kutosha ikiwemo vituo vya kusambaza gesi majumbani ili kuwapunguzia Wananchi gharama ya nishati hiyo.

“Tayari tumesaini  mkataba wa ujenzi wa kituo kikubwa eneo la Mlimani City (Mother station)  kwaajili ya kujaza  gesi asilia  kwenye magari, pia tutajenga vituo vidogovidogo (daughter station) eneo la Muhimbili, eneo la Feri na kiwanda cha madawa Kairuki ili kuongeza kasi ya usambazaji wa gesi hiyo majumbani kwa urahisi zaidi,” amesema Makame.

Aidha, Makame, amewaeleza Wahariri hao wa Habari kuwa milango iko wazi kwa Sekta binafsi kushirikiana na TPDC ili kujenga vituo vingi zaidi vya  kusambaza gesi asilia  Jijini Dar es salaam pamoja na Mikoa mingine.