Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limetajwa kama mpishi anaepika chakula kitamu na kizuri kinachofurahiwa na kupongezwa na wateja ambapo sifa hupewa mhudumu aliyehudumia chakula hicho.

Hayo yamesemwa tarehe 30/05/2023 na Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC Bw. Mussa Makame wakati akimuelezea Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa Majaliwa kuhusu mchango wa TPDC katika kuzalisha umeme unaotumika nchini alipotembelea Banda la TPDC kwenye Maonesho ya Wiki ya Nishati yanayofanyika katika Viwanja vya Bunge Jijini Dodoma.

TPDC imetajwa kuchangia zaidi ya asilimia 70 ya umeme wote unaotumika nchini kupitia gesi asilia.

Maonesho hayo yameandaliwa na Wizara ya Nishati ikiwa ni sehemu ya kutoa nafasi kwa Waheshimiwa Wabunge kujifunza na kujionea utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa na Wizara hiyo kupitia Taasisi zake.

Wizara ya Nishati inatarajiwa kuwasilisha Bajeti yake ya Mwaka 2023/24 Bungeni tarehe 31/05/2023.