Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na kampuni ya TAQA ya nchini Misri wamefikia makubaliano ya kushirikiana katika kufanya utafiti na kuangalia masoko ya gesi asilia katika Mkoa wa Dar es Salaam.

Akizungumza katika hafla hiyo Mkurugenzi wa Idara ya Biashara ya Mafuta na Gesi kutoka TPDC Bw. William Chiome amesema, matokeo ya utafiti huo yatasaidia kuwepo kwa mipango madhubuti ya kusambaza gesi asilia kwa matumizi tofauti.

“Utafiti huu utaenda kufanyika na kukamilika ndani ya mwaka mmoja, na matokeo yake yatawezesha TPDC na makampuni binafsi kujipanga kupeleka miundombinu ya gesi asilia kwa watumiaji mbalimbali sawa na uhitaji ulioonekan,” amesema Chiome.

Kwa sasa kampuni ya TAQA inaendelea na ujenzi wa vituo viwili vya kujazia gesi asilia kwenye magari mkoani Dar es Salaam, vituo vitakavyosaidia watumiaji wa nishati hiyo kuipata kwa urahisi zaidi.