TPDC Yachangia Shilingi Milioni 100 JKCI


Rais mstaafu wa awamu ya nne Dkt.Jakaya Kikwete amezitaka Taasisi na Mashirika kuendelea kuandaa mashindano ya mbio za  hisani (MARATHON) yatakayosaidia katika kuchangisha fedha kwa ajili ya huduma za matibabu kwa wananchi.

Akizungumza  Jijini Dar es salaam kwenye mashindano ya mbio hizo za hisani yaliyoandaliwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC)kwa lengo la   kuwezesha kuchangia gharama za upasuaji kiasi cha Sh.milioni 100 kwa watoto 50 wenye magonjwa ya moyo amesema Serikali imeshafanikiwa kujenga na kuweka mashine za kisasa JKCI zenye gharama ya shilingi bilioni 5 kwa moja hivyo kuwepo mashindano kama haya yataokoa maisha ya watoto wengi walioshindwa kumudu gharama za matibabu.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC Dkt. James Mataragio alisema, pamoja na majukumu yao mengine kurudisha kwa jamii ni jambo muhimu kwao hivyo walianzisha mbio hizo kwa lengo la kuokoa maisha ya watoto wenye matatizo ya moyo ambapo mtoto mmoja hutibiwa kwa Sh.15 milioni.

Aidha Dkt.Mataragio amesema kumekuwepo na mwitikio mkubwa wa  makampuni na watu binafsi katika kushiriki katika mashindano haya hivyo anatamani kuona TPDC Marathon inakuja kiukubwa zaidi katika misimu mwingine ili washiriki waongezeke ambapo itaenda sambamba na ukusanyaji mkubwa wa fedha kwa ajili ya watoto.

Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Profesa Mohammed Janabi alisema kila  mwaka watoto milioni mbili wanazaliwa nchini,asilimia 0.8 mpaka moja wana shida ya moyo na kati yao asilimia 25 wanahitaji upasuaji.

Watoto 511 wanasubiria kupewa huduma ya matibabu ya moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI ), hivyo kuna kila sababu ya kuwachangia ili kuokoa maisha yao.