TPDC Yawaalika Watanzania Kuchangia Matibabu ya Ugonjwa wa Moyo


Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Dkt. James Mataragio amewaomba watanzania kujitokeza kwa wingi kushiriki mbio za hisani maarufu kama TPDC MARATHON zilizoandaliwa na  Shirika hilo kwa lengo la kupata fedha za kusaidia upasuaji kwa watoto 50 wenye matatizo ya moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na Waandishi wa Habari kwenye uzinduzi wa kampeni ya kuhamasisha Wananchi kushiriki katika mbio hizo Dkt. Mataragio amesemea TPDC imeamua kuandaa mbio hizo ili kuwasaidia watanzania na kueleza kuwa mbio hizo zitakuwa endelevu kila mwaka.

Akiwashukuru TPDC na washiriki wengine walioandaa TPDC Marathon  Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Prof. Mohamed Janabi amesema kuwa kila mwaka 1% ya watoto 2,000,000 wanaozaliwa nchini Tanzania sawa na watoto 20,000 huzaliwa na matatizo ya moyo na kati yao 25% sawa na watoto 5,000 wanafanyiwa upasuaji wa moyo katika Taasisi ya Jakaya Kikwete. 

Prof. Janabi ameongeza kuwa kuna watoto 511 wanaosubiri upasuaji hospitalini hapo huku akiahidi kuwa watahakikisha fedha zitakazopatikana zitatumika kikamilifu kwa malengo yaliyokusudiwa na kuongeza kuwa siku hiyo kutakuwa na upimaji wa magonjwa ya moyo bure, utoaji wa chanjo ya Uviko-19 na uchangiaji wa damu kwa hiyari.

Sanjari na hayo Fred Kwezi ambaye ni mratibu wa mbio hizo amewahakikishia washiriki wa mbio hizo kuwa kutakuwepo na huduma zote za kimichezo, kiusalama na kiafya na kuwa usajili unafanyika  kupitia TPDC pamoja na Waratibu wa mbio hizo ambao ni Goba  Road Runners (GRR).

Mbio hizo zenye kauli mbiu isemayo “Kimbia Kwa Afya Yako” zinatarajiwa kufanyika Septemba 11 mwaka huu katika viwanja vya Farasi Oysterbay Jijini Dar es salaam huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete.