Ugunduzi Wa Mafuta Eyasi Wembere Utachochea Ukuaji Wa Uchumi Nchini.


Arusha.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John Mongella alisema endapo Tanzania
itafanikiwa kugundua mafuta katika bonde la Eyasi Wembere Wilayani Karatu
itakuwa ni hatua kubwa na muhimu itakayosaidia kukuza uchumi wa Taifa. 
Mheshimiwa Mongella aliyasema hayo alipokuwa akiongea na Kikosi kazi cha
Maafisa kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) walipofika ofisini
kwake kutoa taarifa ya maendeleo ya mradi. “Mmenipa taarifa kwamba, mradi wa
utafutaji wa mafuta katika bonde la Eyasi Wembere upo katika hatua nzuri, nina
imani kwamba, tukifanikiwa kugundua mafuta katika bonde hili, nchi yetu itapiga
hatua kubwa kiuchumi,” alisema Mhe. Mongella.
Mhe. Mongella alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia
Suluhu Hassan kwa kusaini makubaliano ya awali ya utekelezaji wa mradi wa LNG
utakaofanyika Mkoani Lindi. ’’Tanzania imebarikiwa na Mwenyezi Mungu kwa kuwa
na rasilimali nyingi ikiwemo gesi asilia ambayo iligundulika katika Mikoa ya Kusini,
shabaha ya Rais Samia ni kuhakikisha nchi inapiga hatua kubwa kiuchumi, hasa
Taifa linapokuwa na nishati ya kutosha ya mafuta na gesi asilia,’’alisema Mongella.
Aidha Mongella alisema wao kama Mkoa wa Arusha ambako shughuli hizo za utafiti
zinafanyika Wilayani Karatu, wapo tayari kushirikiana na TPDC ili mradi huo uweze
kukamilika kwa mafanikio makubwa, kwa maslahi mapana ya Taifa.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Karatu Mhe. Dadi Kolimba aliwahakikishia
Ushirikiano, Ulinzi na Usalama timu ya Mradi katika kipindi chote cha shughuli
husika. 
“Napenda kuwahakikishia kwamba, Wilaya itatoa ushirikiano wa dhati ikiwa ni
pamoja na ulinzi na usalama katika kipindi chote cha utekelezaji wa shughuli iliyopo
mbele yenu,” alisema Mh.Kolimba.
Awali, akitoa maelezo ya utangulizi kuhusu mradi, Meneja Mradi kutoka TPDC
Ndugu Sindi Maduhu alisema mradi wa utafutaji mafuta katika bonde la Eyasi
Wembere umepiga hatua kubwa na hatua iliyofikiwa hivi sasa ni ukusanyaji wa
sampuli za kijiokemia zitakazosaidia kupata taarifa za viashiria vya uwepo wa mafuta
au gesi katika eneo husika. 
Katika mwaka wa fedha 2022/23, Shirika limepanga kufanya utafiti wa kijiokemia
(Surface Geochemical Survey) wenye lengo la kukusanya taarifa za viashiria vya
uwepo wa mafuta au gesi asilia katika maeneo mbalimbali nchini.
Maeneo ambayo yametengwa kwa ajili ya utafiti huo yanahusisha Mikoa mitano (5)
ambayo ni Arusha (Karatu), Singida (Iramba na Mkalama), Tabora (Igunga),
Shinyanga (Kishapu) na Simiyu (Meatu).