Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limewezesha ziara ya wanafunzi wa vilabu vya mafuta na gesi asilia kwa shule za Sekondari  Mkoani Mtwara. Ziara hiyo imelenga kuwajengea uwezo wa kutambua rasilimali za mafuta na gesi asilia zilizopo nchini, kuwaandaa wanafunzi kuwa mabalozi wazuri wa kuisemea sekta ya mafuta na gesi asilia pamoja na kuwapa hamasa ya kusoma kwa bidii ili kuwa wataalamu kwenye sekta ya mafuta na gesi asilia nchini hapo baadae.

Akizungumza wakati wa ziara ya wanafunzi 130 kutoka Shule 8 za Wilaya ya Mtwara iliyofanyika Machi 09, 2023 Afisa Maendeleo ya Jamii wa TPDC Bw. Oscar Mwakasege ambaye pia ni Mratibu wa programu ya vilabu vya gesi mashuleni kwa Mikoa ya Lindi na Mtwara alisema TPDC ilianzisha vilabu vya gesi mashuleni kwa shule za sekondari 17 za Mkoani Mtwara ili kuwajengea uelewa wanafunzi wa kutambua rasilimali za nishati ya mafuta na gesi zilizopo nchini pamoja na kuandaa mabalozi wazuri watakao elimisha jamii juu ya rasilimali za gesi na  mafuta nchini.   

Katika hatua nyingine Meneja wa Kiwanda cha kuchakata gesi asilia cha Madimba Mhandisi Sultan Pwaga alisema kuwa, uzalishaji wa gesi asilia umeongezeka hadi kufikia futi za ujazo milioni 105 kwa siku kiwango ambacho ni kikubwa ukilinganisha na awali ambapo futi za ujazo milioni 45 zilizalishwa kwa siku. Aidha alisema kuwa ziara ya wanafunzi hao kwao ni chachu ya kusoma kwa bidii ili waweze kuwa mabalozi wazuri wa kuelimisha jamii na kutunza miundombinu ya gesi asilia nchini.

‘’Kuongezeka kwa uzalishaji wa gesi asilia kumeleta manufaa makubwa kwa nchi ikiwani pamoja na kuchangia kuwa na umeme wa uhakika nchini zaidi ya asilimia 70 kwenye gridi ya Taifa, ukuaji wa sekta ya viwanda na kuokoa fedha za kigeni, kutengeneza wataalamu wa ndani ya nchi kwenye sekta ya gesi asilia ambapo hadi sasa miundombinu ya gesi asilia inasimamiwa na wataalamu wa ndani kwa asilimia 100’’ alisema Pwaga.

Aidha, Pwaga aliongeza kuwa,  rasilimali hii imetutengenezea wataalamu kwenye sekta ya gesi na ni hatua kubwa kama nchi kwani miundobinu hii inaendeshwa na wataalamu wa ndani, vilevile sekta hii inahitaji rasilimali watu na tunahitaji kuzalisha wataalamu zaidi ndio maana TPDC ilianzisha klabu mashuleni kwa lengo la kutoa hamasa kwa wanafunzi ili kuona fursa mbalimbali zinazopatikana katika sekta hii ya gesi ikiwemo  taaluma ya  uhandisi wa aina mbalimbali , wataalamu wa fedha, wataalamu wa utawala,  wataaklamu wa jamii, masijala , kwa hiyo kila fani inayopatikana ndani ya nchi yetu wananafasi ya kutoa mchango kwenye sekta ya gesi.

Kwa niaba ya wanafunzi wenzake, Daudi Kasinje ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Naliendele alisema, ziara ya kutembelea miundombinu hiyo imewapa  hamasa ya  kusoma kwa bidii kwani sekta ya gesi inahitaji taaluma mbalimbali kama Wataalamu wa Fedha, Wahandisi, Wataalamu wa Manunuzi, rasilimali, Maendeleo ya Jamii n.k  

“Nimefurahi kuona kiwanda kikubwa cha kuchakata gesi asilia ambacho kimebeba dhamana kubwa ya nchi ya kuzalisha gesi na ni watanzania pekee wakiendesha mitambo na kuwezesha umeme kuzalishwa. Nimeona kuwa fursa ni nyingi katika sekta ya gesi hivyo uwepo wa klabu hizi utaongeza zaidi hamasa ya kusoma kwa bidii na kuwa na matamanio ya kufanya kazi katika sekta ya mafuta na gesi asilia nchini,” alisema Kasinje.