Waziri Makamba Atoa Maagizo Kwa TPDC Na PURA
Waziri wa Nishati Mhe. January Makamba, ameliagiza Shirika la Maendeleo ya Petroli
Tanzania (TPDC) pamoja na Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA),
kuhakikisha mradi wa uchimbaji wa gesi kitalu cha Ruvuma kilichopo Mkoani Mtwara
unakamilika kwa wakati.
Mhe. Makamba ameyasema hayo leo tarehe 25/11/2022 Jijini Dar es Salaam wakati
halfa ya uwekaji saini Mkataba wa Nyongeza wa Uzalishaji na Ugawanaji Mapato (PSA)
Kitalu cha Ruvuma-Mtwara kati ya Wizara ya Nishati, TPDC, Kampuni ya ARA
Petroleum na Kampuni ya Ndovu Resources.
‘’Dhamira ya Serikali ni kuona mradi huo unakamilika ndani ya miezi 12 hadi 18 na
hatutegemei kusikia mradi huo unachelewa kutokana na changamoto ya fedha.Mradi
huo ukikamilika utakuwa mradi wa kwanza wa gesi ambao utalinufaisha Taifa katika
nyanja mbalimbali ikiwemo Serikali kupata Mrahaba (12.5%) , kupata kodi, Serikali
kupata gawio la mapato yatokanayo na mauzo ya gesi pia ajira kwa Wananchi wa
Mikoa ya Lindi na Mtwara” amesema Mhe. Makamba.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania
(TPDC) Dkt. James Mataragio amesema utafiti na ugunduzi wa gesi ulishafanyika na
kinachofanyika sasa hivi ni kuanza kwa ujenzi wa bomba la gesi kutoka eneo la
Ntorya hadi Madimba na baada ya kukamilika kwa ujenzi huo uzalishaji wa gesi
utaanza.
Dkt. Mataragio amesema kuwa uwekezaji huo wenye thamani ya dola za Kimarekani
milioni 500 unatarajiwa kuzalisha takribani futi za ujazo trilioni 1.6 ambacho ni kiasi cha
gesi kilichogunduliwa katika eneo hilo na kuweka wazi kuwa utekelezaji wake utasaidia
kuongeza chachu na wawekezaji wengi zaidi.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya ARA Petroleum (Tanzania) Ndg. Erhan Saygi
ameishukuru Serikali ya Tanzania hususan Viongozi wa Serikali za Vijiji kwa ushirikiano
waliouonyesha na kuongeza kuwa kukamilika kwa mradi kutachagiza uboreshaji wa
miundombinu na kuongeza ajira ili kukuza pato la wananchi na Taifa kwa ujumla.
Hafla hiyo imehudhuriwa na Viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Lindi Bi.
Zainab Telack, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas Ahmed pamoja na
Wabunge wa Mikoa ya Lindi na Mtwara.