Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) liliendesha zoezi la utoaji elimu kwa Wananchi wa Vijiji/Mitaa inayopitiwa na miundombinu ya gesi asilia.Shirika limekua na utaratibu wa kutoa elimu kwa umma juu ya miradi mbalimbali ya utafiti na uendelezaji wa nishati ya mafuta na gesi asilia nchini. Elimu hii imetolewa ikiwa ni sehemu ya kuimarisha mahusiano mazuri na kuwajengea uwezo wananchi kutambua fursa za uwekezaji wa miradi ya gesi pamoja na kuimarisha ulinzi na usalama wa miundombinu ya bomba la gesi asilia.

Zoezi hilo lilifanyika Mkoani Lindi kupitia mikutano ya hadhara katika Vijiji ambavyo vimepitiwa na mradi wa bomba la gesi asilia ambapo elimu hiyo ilijikita kwenye mada za ulinzi na usalama, fursa zinazoambatana na miradi ya gesi asilia (manufaa) pamoja na Uwajibikaji wa Shirika kwa Jamii (CSR).

Akizungumza katika moja ya mikutano na wananchi wa Kijiji cha Somanga Kusini, Afisa Maendeleo ya Jamii wa TPDC Bw. Oscar Mwakasege alieleza kuwa utunzaji na usalama wa mradi wa bomba la gesi asilia nchini ni pamoja na ushirikishwaji wa wananchi katika ngazi zote hususani katika kupata taarifa, elimu, utekelezaji wa miradi ya kijamii pamoja na ushirikishwaji kwenye ulinzi na usalama.

‘’Mradi wa bomba la gesi asilia umekua na manufaa makubwa kwa jamii na Taifa kwa ujumla ambapo mpaka sasa 70% ya umeme nchini unazalishwa kwa kutumia gesi asilia hivyo kuchagiza  ukuaji wa Sekta mbalimbali, kadhalika gesi asilia inatumika  kuendeshea mitambo viwandani ambapo viwanda vipatavyo 53 na nyumba takribani 1500 za Mikoa ya Dar es salaam, Mtwara na Lindi (Mnazi mmoja) zimeunganishwa  katika mtandao  wa gesi asilia kwa  matumizi ya kupikia majumbani,  aidha mpaka sasa zaidi ya magari 1500 yanatumia gesi asilia kama nishati mbadala wa petroli na dizeli,’’alisema Mwakasege.

Katika hatua nyingine Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Usalama TPDC Bw.Fredy Mfikwa alieleza kuwa mradi wa bomba la gesi asilia umegusa Vijiji na Mitaa 139 kuanzia Msimbati Mtwara hadi Dar es salaam. Aidha, alieleza kuwa TPDC inashirikiana vizuri na Vijiji/Mitaa hiyo kwenye suala la ulinzi na usalama ikiwa ni pamoja na kutoa fedha kila mwezi kwa kila Kijiji/Mtaa ili kuwezesha vijiji hivyo kufanya usafi  kwenye njia (Mkuza) wa bomba la gesi asilia.  

Bw.Mfikwa alitoa rai kwa wananchi kuendelea kuitunza miundombinu ya bomba la gesi asilia kwa kuacha kufanya shughuli hatarishi za kibinadamu ndani ya miundiombinu hiyo, pamoja na kuwasisitiza wananchi kuendelea kutoa taarifa kwa uongozi wa Vijiji/Mitaa au TPDC pindi wanapoona mazingira hatarishi ndani ya miundombinu ya bomba la gesi asilia.

’Shughuli za kibinadamu ambazo hazipaswi kufanywa ndani ya Mkuza wa bomba la gesi asilia kama kuchimba mchanga, kilimo cha mazao ya muda mfupi na mrefu, kuchoma nyasi moto, kupitisha makundi makubwa ya mifugo na shughuli zozote za ujenzi haiziruhusiwi, hivyo natoa rai kwa Uongozi wa Vijiji na wananchi kuendelea kudumisha ulinzi na usalama ili bomba hilo liendelee kuwa na manufaa kwa sasa na baadae,’’ alieleza Mfikwa.